Luke 12

Maonyo Dhidi Ya Unafiki

(Mathayo 10:26-33)

1 aWakati huo, umati mkubwa wa watu maelfu, walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Isa akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao. 2 b cHakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana. 3Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonong’ona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.

4 d“Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi. 5 eLakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo! 6Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao. 7 fNaam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

8 g“Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. 9 hLakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu. 10 iNaye kila atakayenena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11 j“Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema. 12 kKwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Mfano Wa Tajiri Mpumbavu

13Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Isa, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”

14 lLakini Isa akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” 15 mNdipo Isa akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

16Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

18“Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 nNami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’

20 o“Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

21 p“Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

Msiwe Na Wasiwasi

(Mathayo 6:25-34)

22 q rKisha Isa akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. 23Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. 24 sFikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! 25Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? 26Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

27 t“Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 28 uBasi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! 29Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. 30 vWatu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 31 wBali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.

Utajiri Wa Mbinguni

(Mathayo 6:19-21)

32 x“Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 yUzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 zKwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

Kukesha

35 aa“Kuweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka, 36 abkama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka kwenye karamu ya arusi, ili ajapo na kubisha mlango waweze kumfungulia mara. 37 acHeri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia. 38Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja mnamo usiku wa manane, au karibu na mapambazuko. 39 adLakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angalijua saa mwizi atakuja, asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. 40 aeNinyi nanyi hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.”

Mtumishi Mwaminifu Na Yule Asiye Mwaminifu

(Mathayo 24:45-51)

41Ndipo Petro akamuuliza, “Bwana, mfano huu unatuambia sisi peke yetu au watu wote?”

42 afIsa akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya watumishi wake wote, ili awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa? 43Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44 agAmin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 45 ahLakini kama yule mtumishi atasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike, na kula na kunywa na kulewa. 46 aiBasi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wale wasioamini.

47 aj“Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48 akLakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.

Isa Kuleta Mafarakano

(Mathayo 10:34-36)

49 al“Nimekuja kuleta moto duniani; laiti kama ungekuwa tayari umewashwa! 50 amLakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu mpaka ubatizo huo ukamilike! 51 anMnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano. 52 aoKuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. 53 apWatafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, naye mama mkwe dhidi ya mkwewe na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”

Kutambua Majira

(Mathayo 16:2-3)

54 aqPia Isa akauambia ule umati wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha. 55Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo. 56 arEnyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa?

57“Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki? 58 asUwapo njiani na mshtaki wako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani. 59 atNakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.”
Copyright information for SwhKC